Top News

 

        

Katibu Mkuu CCM ampongeza Mkandarasi Mradi wa SGR kutatua changamoto iliyokuwepo Mto Mkondoa.

Na Antony Sollo  - Kilosa.

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo amefanya ziara ya kutembelea Stesheni ya Reli ya kisasa,iliyoko Kilosa Mkoani Morogoro katika kipande cha pili cha Mradi wa Ujenzi wa Reli ya kisasa SGR, Morogoro – Makutupora iliyofanyika Januari 30 mwaka huu.

Stesheni ya Reli ya SGR iliyoko Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro ni moja kati ya vituo vya ziara ya Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo ziara yenye lengo la kuwatembelea wananchi na kusikiliza changamoto zao ili kuzitafutia ufumbuzi.

Akiwa stesheni ya SGR Kilosa, Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo ameeleza kuwa ujenzi wa reli ya kisasa umeleta ufumbuzi wa kero ya muda mrefu ya miundombinu ya Reli kusombwa na maji kipindi cha mvua.

“Kilosa lilikuwa ni eneo ambalo Reli ya kati inapata madhara makubwa hasa mvua ikinyesha,hii ni kutokana na mto Mkondoa ambao ulikuwa unaathirika sana kuliko mahali popote, lakini sasa ni tofauti kutokana na Miundombinu hii bora na ya kisasa niwapongeze wakandarasi kwa kazi nzuri”alisema Katibu Mkuu Chongolo.

Stesheni ya SGR ya Kilosa ni moja kati ya vituo vya kati vya Reli hiyo,ambacho kinategemewa kuhudumia wananchi wa Wilaya ya kilosa na maeneo jirani ukiwemo Mkoa wa Iringa na kupitisha watalii kuelekea Hifadhi ya Taifa ya Mikumi.

Akitoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa Reli ya kisasa Mkurugenzi Mkuu wa TRC Masanja Kadogosa, alisema kuwa hadi sasa ujenzi wa Reli hiyo unaendelea vizuri ambapo kipande cha Dar es salaam – Morogoro kimefikia zaidi ya 97%, kipande cha Morogoro – Makutupora zaidi ya 91%, Makutupora – Tabora 3.95%, Tabora – Isaka 1% na kipande cha Mwanza – Isaka zaidi ya 22.7%.

Aidha Mkurugenzi Mkuu Kadogosa alisema kuwa Ujenzi wa Reli ya kisasa utakapokamilika utakuwa na manufaa makubwa katika Sekta ya Biashara na uwekezaji, ambapo katika kipindi cha ujenzi, awamu mbili za ujenzi wa SGR zitatengeneza zaidi ya ajira 40,000 huku thamani ya dhabuni zilizotolewa kwa wakandarasi wa ndani zikifikia zaidi ya shilingi Trilioni 1.8.

Aidha Katibu Mkuu Daniel Chongolo ameipongeza Serikali kwa utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Reli ya kisasa kwa lengo la kuwaletea maendeleo watanzania.

“Nimpongeze Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka kipaumbele katika kuhakikisha Ujenzi wa Reli hii unafanyika kwa kasi lakini kwa vipande vingi vinavyounganisha Dar es salaam hadi Mwanza na Dar es Salaam hadi Kigoma”alisema Chongolo.

Katika ziara hiyo,Mbunge wa Kilosa Prof. Paramagamba Kabudi, Mbunge wa Mikumi Denis London na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Shaka Hamdu Shaka walihudhuria.

Aidha  Katibu Mkuu wa CCM Dainiel Chongolo amesisitiza juu ya umuhimu wa kulinda miundombinu ya Reli kwa manufaa ya taifa kwa ujumla.

 

 

 

 

Post a Comment

Mpya zaidi Nzee zaidi