Top News

 

Madiwani matatani kwa kukipaka Matope CCM.

Na Antony Sollo  KAHAMA.

MADIWANI wa Kata ya Nyahanga Manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga Panklasi Ikongoli na Helena Bundala wanatuhumiwa kumpa vitisho Askofu Mkuu wa Kanisa la Mlima wa Makimbilio (HMM) Riziki Esromu Makanika baada ya kwenda katika eneo ambalo Askofu huyo alilinunua kwa ajili ya shuhghuli mbalimbali za kijamii.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Askofu Mkuu wa Kanisa la Makimbilio Riziki Esromu alisema kuwa baada ya kununua maeneo hayo akiwa anayaendeleza kila mwaka kwa kupanda miti na mazao ya muda mfupi kama mpunga ndipo Madiwani hao wawili Panklas Ikongoli na yule wa Viti Maalumu Helena Bundala walifika na kulazimisha kupatiwa viwanja vinne ili wavimiliki.

Hata hivyo baada ya ombi hilo kugonga mwamba wawakilishi hao wa wananchi kupitia Chama cha Mapinduzi walimpa vitisho Askofu huyo kuwa kwa kuwa amegomea ombi lao watakwenda kusimika bendera ya Chama cha Mapinduzi katika maeneo yake ili anyang’anywe kwa kupitia mgongo wa Chama.

Askofu Mkuu wa Kanisa la Makimbilio Riziki Esromu alinunua maeneo hayo mwaka 2011 kutoka kwa watu tofauti tofauti katika eneo lililoko Mtaa wa Mtakuja amblo kabla ya mabadiliko ya Kiutawala lilikuwa Kijiji cha Shunu Kitongoji cha Kagera.

Gazeti hili limeweza kupata Nakala za vielelezo vinavyothibitisha umiliki wa maeneo hayo kutoka kwa wananchi kwenda kwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Makimbilio ambapo baada ya kutaka kujiridhisha Mwandishi wa Habari alimtafuta Diwani Helena Bundala ili kutolea ufafanuzi juu ya tuhuma hizo.

Akizungumza na gazeti hili Diwani huyo aliruka futi elfu kumi na kudai kuwa hana taarifa za uwepo wa Mgogoro katika eneo hilo.

“sina taarifa za kuwepo kwa Mgogoro baina yangu na Askofu huyo na sijawahi kwenda kwake kuomba eneo hivyo taarifa hii ni ngeni kwangu”alisema Bundala.

Hata hivyo gazeti hili limeshuhudia baadhi ya jumbe fupi za simu za mkononi wakiwasiliana na Askofu Mkuu wa Kanisa la Makimbilio kuhusiana na kutaka kupatiwa maeneo ambapo baada ya kusikika kuwa suala hilo linafuatiliwa na waandishi wa Habari ameamua kujiweka pembeni.

Katika mwendelezo wa vitisho alivyopatiwa Askofu huyo ushahidi umeonyesha kuwa yale waliyoyasema ni kweli Madiwani hao walimpandikiza mtu aliyejulikana kwa jina la Stephen Joseph Kafumu ambaye aliwahi kuwa Mwenyekiti Mstaafu wa chama cha Mapinduzi Kata ya Nyahanga kuwa mmiliki wa eneo hilo ambaye hata hivyo hana nyaraka yoyote kuthibitisha umiliki wa eneo hilo.

Akizungumzia Sakata la kutishiwa na Madiwani hao Askofu Mkuu wa Kanisa la Makimbilio Riziki Esromu Makanika alisema kuwa akiwa katika Ofisi ya Mwenyekiti wa Mtaa wa Mtakuja Julius Sabuni Disemba 19 . 2022 baada ya mahojiano alipoulizwa kama ana nyaraka yoyote inayoweza kuchukuliwa kama ushahidi kwa ajili ya kuthibitisha umiliki wake wa eneo alisema hana bali eneo hilo ni la ukoo.

Gazeti hili lilimtafuta Diwani wa Kata ya Nyahanga Panklasi Ikongoli ili kutolea ufafanuzi tuhuma za kutoa vitisho kwa Askofu wa Kanisa la Makimbilio alisema kuwa hawezi kuzungumza chochote kutokana na kwamba hayuko katika maeneo mazuri kuzungumza.

“sitaweza kuzungumza chochote njoo Ofisini tuzungumze kwa nini usije?leo ni siku ya mapumziko leo siwezi kuzungumza,ukipata nafasi njoo Ofisini”alisema Ikongoli.

DIWANI AFUNGA OFISI YA BARAZA LA  KATA NYAHANGA.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa baada ya kukosekana kwa ushahidi kutoka kwa Stephen Kafumu ambaye alitengenezwa na Diwani huyo kuwa ni mmiliki wa eneo hilo Diwani Ikongoli aliamua kufunga Ofisi za baraza la Ardhi la Kata ili kupinga kutolewa kwa Hati ya kushindwa kusuluhisha ili mlalamikaji asiende mbele.

“Ndugu mjumbe wa baraza la Kata ya Nyahanga pokea taarifa kwamba baraza limesimamishwa rasmi kuanzia leo tarehe Disemba 28 2022 hadi hapo mapema januari 2023 kikao cha WDC kitakapokaa wasiliana na WEO kwa Utekelezaji”ilisema sehemu ya ujumbe huo ambao ulisambazwa kwa wajumbe wa baraza hilo.

Gazeti hili lilimtafuta Mwenyekiti wa CCM Kata ya Nyahanga Lucas Matanyanga ili kutolea ufafanuzi kuhusiana na tuhuma dhidi ya Madiwani hao ambapo alikiri kupokea malalamiko na kusema Ofisi yake inafanyia kazi na ikikamilisha na kubaini ukweli itachukua hatua stahiki.

“Ni kweli Ofisi yangu ya Chama cha Mapinduzi  imepokea malalamiko kuhusu Mgogoro huo,Ofisi yangu inafanyia kazi na ikikamilisha na kubaini ukweli tutachukua hatua stahiki”alisema Matanyanga.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Kahama Thomas Muyonga ili kuzungumzia Sakata la Madiwani wa Kata ya Nyahanga kutoa Vitisho kwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Makimbilio Riziki Esromu Makanika ambapo alisema hana taarifa juu ya malamiko hayo lakini akasema Chama cha Mapinduzi hakina utaratibu wa kupora maeneo ya watu badala yake kinatetea wananchi kwa maslahi mapana ya kulinda Amani na Utulivu kwenye jamii.

Kuhusu suala la Madiwani hao kuanzisha mgogoro baina ya watumishi wa Mungu kwa kivuli cha chama Mwenyekiti huyo alisema iwapo itabainika kuwepo kwa matumizi mabaya ya jina la Chama chama hakitasita kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya Madiwani hao.

“Chama cha Mapinduzi hakina utaratibu wa kupora maeneo ya watu badala yake kinatetea wananchi kwa maslahi mapana ya kulinda Amani na Utulivu kwenye jamii,kuhusu suala la Madiwani hao kuanzisha mgogoro baina ya watumishi wa Mungu kwa kivuli cha chama Mwenyekiti huyo alisema iwapo itabainika kuwepo kwa matumizi mabaya ya jina la Chama chama cha Mapinduzi hakitasita kuchukua hatua za kinidhamu kwa mujibu wa Kanuni za Chama dhidi ya Madiwani hao”alisema Mwenyekiti wa CCM Kahama.

Pichani ni Askofu Mkuu wa Kanisa la Mlima wa Makimbilio (HMM) Riziki Esromu Makanika akionyesha mawe yaliyowekwa na baadhi ya watu waliouziwa viwanja na Madiwani wa Kata ya Nyahanga ambao wanadaiwa kumtishia Askofu huyo Picha na Antony Sollo.

 

 

Post a Comment

Mpya zaidi Nzee zaidi