JWTZ yatoa siku saba kwa wananchi,wafanyabiashara nchini kusalimisha Sare za Jeshi.
NA ANTHONY SOLLO - DODMA
JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania limetoa muda wa siku saba kwa wananchi na wafanyabiashara kusalimisha mavazi ya Jeshi au yale yanayofanana na Sare za Kijeshi.
Akizungumza na vyombo vya Habari katika Ukumbi wa Habari Maelezo Jijini Dodoma,
Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano Makao Makuu ya Jeshi la Wananchi (JWTZ) Luteni Kanali Gaudentius Gervas Ilonda amesema kuwa Jeshi hilo limeshtushwa na kuwepo kwa wimbi kubwa la baadhi ya Wananchi au kuonekana wamevaa Sare za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania ikiwemo mavazi yanayofanana na Sare za Kijeshi.
"Tumekutana hapa leo ili kupitia kwenu JWTZ liweze kutoka ufafanuzi kwa jamii ya Watanzania (wananchi) kuhusiana na kadhia hiyo inayokinzana na katazo la Sheria linalokataza raia kuvaa kumiliki au kuuza mavazi ya Kijeshi au yanayoelekea kufanana na Sare za Kijeshi" alisema Leteni Ilonda.
Kwa mujibu wa Kanali Ilonda mavazi yanayokatazwa kuvaliwa ni pamoja na Kombati (vazi la mabaka mabaka) makoti,Tisheti,Suruali,Magauni,Kofia,Viatu,mabegi,na kaptula wenye rangi zinazofanana au kushonwa katika mtindo ya Kijeshi.
Akiifafanua kuhusu katazo Luteni Ilonda alisema kuwa katazo hilo ni kwa mujibu wa Kifungu cha 99 cha Sheria ya Ulinzi wa Taifa (NDA) sura ya 192 ,Sheria namba 24 ya 1966 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002.
Aidha Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano Makao Makuu ya Jeshi la Wananchi (JWTZ) Luteni Kanali Gaudentius Gervas Ilonda alisema kuwa Kifungu cha 178 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sure ya 16 (penal code) na Kifungu cha 6 cha Sheria ya Usalama wa Taifa vinakataza Raia kuvaa Sare na mavazi ya majeshi ya Ulinzi au yanayofanana nayo.
Kanali Gaudentius Gervas Ilonda alisema kuwa wapo baadhi ya Watu ambao kwa kutumia mavazi hayo wamekuwa wakiwatapeli wananchi huku wengine wakitumia kufanya vitendo vya kihalifu huku wakodhaniwa kuwa ni wanajeshi.
"Vitendo vya matumizi ya mavazi ya Kijeshi ni uvunjifu wa Sheria za nchi hivyo havipaswi kufumbiwa macho na hali hii ikiachwa kuendelea unaweza kuhatarisha Ulinzi na Usalama wa nchi yetu"alisema Luteni Ilonda.
Hata hivyo Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano Makao Makuu ya Jeshi la Wananchi (JWTZ) Luteni Kanali Gaudentius Gervas Ilonda alisema kuwa zipo taasisi zinazowashonea watumishi wake Sare za aina hiyo wakiwemo wafanyabiashara wanaoingiza nchini mavazi ya aina hiyo na kuyauza kwa baadhi ya raia kupitia katika maduka au maeneo yao ya biashara.
Katika hatua nyingine Luteni Ilonda aliwataka wasanii wanaovaa mavazi hayo na kuyatumia wawapo kwenye majukwaa ya kazi zao bila kufuata utaratibu wafuate Sheria kwa kuomba vibali ili waweze kutumia mavazi na kwamba iwapo hawatatekeleza hatua kali zitachukuliwa.
Luteni Kanali Gaudentius Gervas Ilonda alisema kuwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania JWTZ litaendelea kudumisha ushirikiano na mshikamano na Wananchi ili kuweza kutimiza jukumu lake kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Chapisha Maoni