NA ANTHONY SOLLO - SHINYANGA
WACHIMBAJI wadogo wa Madini wanaomiliki Leseni ya Uchimbaji wa Madini katika Mgodi wa Mwakitolyo Namba 5 ujulikanao kwa jina la MGM ulioko Halmashauri ya Shinyanga Mkoani Shinyanga wametenga zaidi ya Sh Mil 11.886 kwa ajili ya kupambana na majanga ya mvua kufuatia utabiri uliotolewa na Mamlaka ya hali ya hewa nchini TMA.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa Habari waliotembelea Mgodini hapo kujionea namna wachimbaji wanavyojiandaa na tishio la mvua za Elinino nchini ,Meneja Msaidizi wa Mgodi wa Mwakitolyo Gold Mine MGM,Matemla Michael alisema uamuzi huo umetokana na maelekezo yaliyotolewa na Nov 23 na Waziri wa Madini Wakili Msomi Anthony Mavunde ambaye alifanya ziara Mkoani Shinyanga na baadaye kutembelea katika Mgodini hapo.
Kwa mujibu wa Meneja Matemla,akiwa Mgodini hapo Waziri wa Madini Wakili Msomi Anthony Mavunde aliwaelekeza wachimbaji hao kutengeneza mitaro ya maji katika eneo la Mgodi huo ili kuhakikisha maji yanapata uelekeo sahihi na kuepusha madhara ambayo yangeweza kusababisha vifo kwa wachimbaji na wananchi kwa ujumla.
Meneja Matemla alibainisha kuwa,katika zoezi linalofanywa na Mgodi huo la kuchimba na kusawazisha Ardhi kuepusha majanga wameweza kuokoa duara zaidi ya (110) ambazo zingeathirika na maji na kusababisha zaidi ya wachimbaji (660 ) kukosa Ajira.
Katika hatua nyingine Meneja Matemla alianika mafanikio lukuki yaliyofikiwa na wachimbaji hao katika shughuli zao tangu Serikali iwapatie Leseni ya uchimbaji mwaka 2019 ambapo mpaka sasa Mgodi huo umefanikisha kulipa Mapato ya Serikali zaidi ya Sh Mil 620 huku wakishiriki shughuli mbalimbali za Kijamii na Kitaifa.
Kufuatia gharama kubwa wanazotumia kwa ajili ya kufanya ukarabati wa Maduara hayo Meneja Matemla ameeleza matamanio ya wachimbaji wa kikundi hicho ya kumiliki mashine na mitambo ya uchimbaji na uchenjuaji wa Madini ili kuongeza Mapato na pia waweze kutimiza ndoto yao ya kuongeza kipato chao pamoja na kuisadia Serikali na jamii ya watanzania kufanyia matengenezo ya miundombinu ya barabara katika maeneo mbalimbali wanapofanyia shughuli zao.
“Kama wachimbaji tunatamani sana kumiliki mashine na mitambo ya kisasa kwa ajili ya kuboresha uchimbaji na uchenjuaji wa Madini ili kuweza kuongeza Mapato ili tuweze kutimiza ndoto yetu ya kujipatia mapato pamoja na kuisadia Serikali na jamii ya watanzania kufanyia matengenezo ya miundombinu ya barabara,lakini pia tuiombe Serikali itambue mchango wetu wa Maendeleo kwa Umma”alisema Matemla.
“ Nampongeza sana Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kufanya uteuzi unaokidhi matakwa ya wachimbaji kwa kumteua Wakili msomi Anthony Mavunde kuwa Waziri wa Madini,Waziri huyu ni msikivu,mfuatiliaji,na ni mkweli hivyo sisi wachimbaji tuna Imani naye”alisema Meneja Matemla.
Akielezea mafanikio yaliyopatikana na yanayoinufaisha jamii moja kwa moja Meneja Matemla alisema mpaka sasa Mgodi umefanikiwa kununua gari la wagonjwa Toyota Hiece lenye thamani ya Sh Mil 60,ujenzi wa vyumba vya Madarasa matatu yenye hadhi Mil 68,Ujenzi wa Soko la Madini ambapo Mgodi huo umechangia Sh Mil 7,awamu ya pili ya ujenzi wa vyumba vya Madarasa na Ofisi jumla ya Sh Mil 26,na ujenzi wa vyumba vya Madarasa Shule ya Sekondari Mwakitolyo Mil 8.
Michango mingine ni pamoja na ujenzi wa Jengo la Kituo cha Polisi tofali 100 zenye thamani ya Sh 230,000,ujenzi wa jengo la Utawala CCM Wilaya ya Shinyanga Vijijini Mil 1,pamoja na ushiriki katika shughuli mbalimbali za Kijamii na Kitaifa.
Kuhusu lengo mahsusi la Uongozi wa Mgodi huo Meneja Matemla alisema,mgodi huo umedhamiria kuendeleza wachimbaji (wanachama)kwa kuwapatia fedha za kuendeleza maduara yao hasa pale wanachama hao wanapopata changamoto ya kiuchumi na kupelekea kushindwa kuendeleza shughuli za uchimbaji.
“Sisi kama uongozi wa Mgodi tunawathamini na kuwapenda sana wanachama wetu kwani tunatambua juhudi na michango yao katika kupatikana mapato tunayojivunia hivyo pale wanapokwama sisi tunawapa nfedha ili waweze kupambana na hali mbaya kiuchumi na kufanmikisha maelengo yao na hili ni jukumu letu”alisema Meneja Matemla.
Hata hivyo Meneja Matemla
ameiomba Serikali iharakishe mchakato wa kuwafanya wachimbaji watambulike na
Taasisi za fedha ili waweze kukopesheka kwa masharti nafuu maana bila hivyo
shughuli zao haziwezi kuwa bora na wataendelea kushuka kimapato jambpo ambalo
linaweza kuathiri uchumi na pato la Taifa.
Naye Meneja Mkuu wa Mgodi wa MGM
(Mwakitolyo Gold Mine)Leonard Waziri
alisema Uongozi wa Mgodi huo umeanzisha Mradi wa wachimbaji wadogo kwa
ajili ya kuondoa kero kwa wachimbaji kuchangia shughuli mbalimbali ambapo kwa
sasa wamefanikiwa kutengeneza Mwalo ambao ni wa kisasa zaidi na kueleza kuwa
tangu kuanzishwa kwake wameweza kuzalisha kilo 4 za dhahabu na kuweza kupata
kiasi cha zaidi ya Sh Mil 400 ambazo kati ya fedha hizo zimetumika kwa ajili ya
maendeleo ya jamii na kiasi kingine kikibakia kwa ajili ya kusaidia wachimbaji
wenyewe.
“Tumefanikiwa kutengeneza Mwalo
ambao ni wa kisasa zaidi ,tangu kuanzishwa kwake tumeweza kuzalisha kilo 4 za
dhahabu na kuweza kupata zaidi ya Sh Mil 400 ambazo kati ya fedha hizo
zimetumika kwa ajili ya maendeleo ya jamii na kiasi kingine kikibakia kwa ajili
ya kusaidia wachimbaji wenyewe,hay ani mafanikio makubwa,na niwaambie waandishi
wa Habari,Mgodi wa Mwakitolyo Namba 5 ni Mgodi pekee ambao unampunguzia mzigo
wa michango mchimbaji kwa kuchangia 1% pekee ya mapato yake”alisema Meneja Leonard Waziri.
Meneja Mkuu wa Mgodi wa MGM
Mwakitolyo Gold Mine aliiomba Serikali hususani Halmashauri
ya Shinyanga Vijijini na Halmashauri ya Msalala Wilayani Kahama kupitia Wakala
wa Barabara za Mijini na Vijijini TARURA kuzisimamia kikamilifu matengenezo ya
dharura ya barabara za Mwakitolyo Kahama na Mwakitolyo Shinyanga ambazo
zinahusika Zaidi na uchumi wa Halmashauri hizo pamoja na Mkoa wa Shinyanga kwa
ujumla.
“Niiombe sana Serikali yetu
tukufu,iweze kuzisimamia barabara zetu zote zinazohusisha Halmashauri ya
Shinyanga Vijijini na Halmashauri ya Msalala Wilayani Kahama kupitia Wakala wa
Barabara za Mijini na Vijijini TARURA kuzisimamia kikamilifu barabara za
Mwakitolyo Kahama na Mwakitolyo Shinyanga ambazo zinahusika Zaidi na uchumi wa
Halmashauri hizo pamoja na Mkoa wa Shinyanga kwa ujumla,barabara hizi kwa sasa
zinatishia uchumi wa wachimbaji na mawasiliano baina ya jamii ya upande mmoja
kwenda upande mwingine na hali hii itaweza kuathiri uchumi wa wananchi na hasa
wachimbaji”alisema Meneja Leonard Waziri.
Akizungumzia ushiriki wa
wanawake,Justina Bundala Mwanamke pekee aliyejizolea Tuzo lukuki kuhusiana na
Tasnia ya Madini Mkoani Shinyanga na Kitaifa,alimshukuru
Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwapa kipaumbele wanawake katika Sekta ya
Madini kwani amefarijika kuwa mmoja wa wanawake nguli waliojizolea Tuzo
mbalimbali kupitia Sekta ya Madini.
“Namshukuru sana Rais Dkt Samia
Suluhu Hassan kwa kutupa fursa na kipaumbele sisi wanawake katika Sekta ya
Madini,nimefarijika sana kwa kuwa mmoja wa wanawake nguli tuliojizolea Tuzo mbalimbali
kupitia Sekta ya Madini,na ombi langu kwa Serikali,tunaomba Wizara ya Nishati
iboreshe miundombinu ya Umeme kwani ndiyo tegemeo la wachimbaji wadogo kwa
ajili ya kuzalisha Zaidi na kuongeza mapato ya Serikali na pato la mtu mmoja
mmoja”alisema Bundala.
Kwa Habari na Matukio mbalimbali endelea kufuatilia Mtandao huu kwa Habari Makini zilizohakikiwa..........



Chapisha Maoni