Watendaji wa Serikali na wananchi
watekeleza Agizo
la DC
NA ANTHONY SOLLO MBOGWE.
KUFUATIA Mlipuko wa Magonjwa ya kuhara na kutapika kuripotiwa katika moja ya Tarafa za Wilaya ya Mbogwe Mkoani Geita lililotolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe Sakina Mohamed,wananchi wa maeneo mbalimbali katika Tarafa ya Masumbwe kwa kushirikiana na watendaji wa Serikali wameendelea na zoezi la Usafi wa Mazingira kuunga mkono juhudi za Serikali ili kupambana na Magonjwa hayo.
Hivi karibuni Mkuu wa Wilaya
ya Mbogwe Sakina Mohamed aliitisha kikao cha Dharula na kuwataka watendaji wa
Serikali kwenda kutoa Elimu ya namna ya kukabiliana na mlipuko wa magonjwa hayo
kwa wananchi wa makundi mbalimbali.
Akizungumza na waandishi wa
Habari kwa njia ya Simu Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe Sakina Mohamed alikiri kuwepo
kwa taarifa za mlipuko ndani ya Tarafa ya Masumbwe Wilaya ya Mbogwe Mkoani
Geita na kuitisha kikao cha dharula na kutoa maelekezo kwa watendaji wa
Serikali kwenda kutoa Elimu ya namna ya kukabiliana na mlipuko wa magonjwa hayo.
“Mara baada ya kupata taarifa nilichukua hatua za haraka na kukaa Kikao na watendaji wa Serikali,nimetoa maelekezo ya kusambaza tahadhari juu ya uwepo wa mlipuko wa magonjwa hayo na kuwataka watendaji hao kwenda kutoa Elimu kwa wananchi wote kuzingatia kanuni za Afya na matumizi sahihi ya vyoo”alisema DC Sakina Mohamed.
Kwa upande wake Ofisa Madini Mkazi Mkoa wa Kimadini wa Mbogwe Eng Jeremia Hango alipotafutwa na waandishi wa Habari ili kufahamu namna Ofisi yake ilivyojipanga kuhamasisha mapambano dhidi ya ugonjwa wa mlipuko alisema tayari ameshatuma Maofisa wa Madini kwenda katika maeneo yote ya Migodi kwa lengo la kutekeleza maelekezo ya Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe.
“Sekta ya Madini ni kubwa na ina wadau wengi,na mimi kama Ofisa Madini niliyepewa jukumu la kusimamia Sekta hii,baada ya kupokea maelekezo ya Mkuu wa Wilaya tayari nimeshatuma Maofisa wangu wa Madini kwenda kwenye Migodi mbalimbali katika Mkoa wetu wa Kimadini wa Mbogwe kwa lengo la kutekeleza maelekezo ya Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe kutoa Elimu na kuhamasisha wananchi na wachimbaji kuzingatia Kanuni za Afya na matumizi sahihi ya vyoo” alisema Eng Hango.
Akizungumza na Waandishi wa habari Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe Dr. Zakayo Sungura aliitaja Tarafa ya Masumbwe kuwa ndiyo iliyoripotiwa kuwa na wagonjwa wa kuhara na kutapika ambapo mpaka sasa kimeripotiwa kifo cha mtu mmoja kati ya watu saba wenye dalili za ugonjwa huo.
“Ni kweli tumepokea kesi saba za watu walio na dalili za ugonjwa wa kuhara na kutapika zilizoripotiwa katika Kituo cha Afya Masumbwe na mmoja wa wagonjwa hao alifariki wakati akipatiwa matibabu katika Kituo cha Afya Masumbwe”alisema Dr Sungura.
Katika taarifa yake kwa waandishi wa Habari,Dr Sungura alibainisha kwamba wagonjwa waliobainika na dalili za ugonjwa huo wametokea katika maeneo ya Shinyanga “B” huku ikielezwa kuwa maeneo yaliyoathirika zaidi kuwa ni Tarafa ya Masumbwe.
Akitoa takwimu za kuenea kwa ugonjwa huu Dr Sungura alisema hajapata kesi yoyote kutoka katika maeneo ya Tarafa zingine lakini tayari kikao cha dharula kimekaa chini ya Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe Sakina Mohamed na kutoa maelekezo ya namna ya kukabiliana na ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa Dr Sungura wameanzisha Kampeni ya uhamasishaji matumizi ya vyoo na kufanya msako kubaini familia ambazo hazina vyoo na wakibaini wahusika watachukuliwa hatua kali.
“Baada ya kutokea kwa mlipuko huu tumefanya kikao na Mkuu wa Wilaya pamoja na watendaji wa Serikali na kwamba tumepokea maelekezo ya namna tuakavyofanya kazi kama timu ili kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa huu”alisema Dr Sungura.
Katika hatua nyingine Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe Dr Zakayo Sungura aliwataka Watumishi wanaofanya kazi katika Migodi kujisaidia kwenye vyoo kuliko kujisaidia vichakani,kuchemsha maji ya kunawa,kutunza Mazingira kwa kufanya usafi kuandaa chakula katika mazingira safi.
Ili kukabiliana na mlipuko huo Dr Sungura alisema baada ya kuona namna ambavyo maandalizi ya pombe za kienyeji hayaridhishi tayari wamefungia Vilabu vyote vya pombe za kienyeji na juice za miwa kutokana na maandalizi duni yanayoweza kusababisha athari kwa watumiaji.
Akitoa ufafanuzi huo Dr. Sungura alisema kesi ya kwanza ya mlipuko wa ugonjwa huu, mgonjwa wa kwanza iliripotiwa tarehe 1.01.2024. na kuongeza kuwa mpaka sasa hakukuwa na mgonjwa mpya aliyeonekana na dalili za ugonjwa huo na kuwaomba wananchi wote katika Wilaya ya Mbogwe kuchukua tahadhari wakati wa kuandaa chakula akiwataka wachemshe maji ya kunawa na hata yale ya kuoga na kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima alisema Dr Sungura.
Waandishi wa Habari walitembelea Mgodi mama wa Isanjabadugu ulioko Nyakafuru Wilaya ya Mbogwe Mkoani Geita ili kujionea utekelezaji wa agizo la Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe Sakina Mohamed ambapo walikuta wananchi wakifanya usafi katika maeneo yao hii ikiwa ni maandalizi ya kupambana na mlipuko wa magonjwa hayo.
Akizungumza na Vyombo vya Habari Ofisini kwake,Mwenyekiti wa Mgodi wa Isanjabadugu Vicent Maige alisema Uongozi wa Mgodi umepokea maelekezo ya Mkuu wa wilaya na kuanza kufanyia kazi mara moja ili kukabiliana na mlipuko wa magonjwa hayo.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti
huyo,taarifa hizi za mlipuko wa magonjwa ya kuhara ziliwafikia rasmi tarehe
4.01.2024,kupitia kwa Ofisa Afya wa Wilaya pamoja na Ofisa Mazingira wa Wilaya
ya Mbogwe,walituelekeza namna ya kufanya kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa
huo na kusema wao kama uongozi wa Mgodi wamejipanga vizuri kwamba kwa kutambua ugonjwa
wa kuhara unaua watu wengi kwa mpigo kwa hiyo wamechukua tahadhari kubwa kama
walivyoelekezwa kwa kumfikia kila mtu yalipo makazi ya watu.
Kwa upande wa vyoo Mwenyekiti
huyo alibainisha kuwa watu wanaoishi katika eneo hilo ni zaidi ya 800,na Idadi
ya vyoo katika eneo hilo imegawanyika katika sehemu mbili likiwemo eneo
wanalofanyia kazi za Uchimbaji ambapo idadi ya vyoo ni saba (7) na katika eneo
wanalokaa wachimbaji pamoja na watu wengine wanaoingia na kutoka kuna vyoo 150.
Aidha Mwenyekiti huyo
amebainisha kwamba kama wamiliki wa Leseni jukumu walilo nalo ni kuhamasisha
wananchi kuchemsha maji ya kunywa na kunawa mikono pindi wanapotoka chooni
ikiwemo na kuepuka kula vyakula vilivyopoa.

Chapisha Maoni