MADIWANI MSALALA:Tumeridhishwa na Utendaji wa RUWASA katika Miradi ya Maji.
NA ANTHONY SOLLO KAHAMA.
pichani ni muonekano wa Jengo la Kisasa la Halmashauri ya Msalala Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga.
BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Msalala Wilaya Kahama Mkoani Shinyanga limependekeza na kupitisha matumizi ya bajeti ya Sh Bil 10.2 kwa Wakala wa Maji safi na Usafi wa Mazingira RUWASA katika halmashauri hiyo ili kukamilisha utekelezaji wa Miradi mbalimbali inayojengwa na Wakala hiyo.
Akizungumza katika kikao cha
baraza la Madiwani kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Msalala Khamis Katimba amesema kuwa,kutokana na michango
ya Madiwani ndani ya Kikao cha baraza hilo ni ishara tosha kwamba wameridhishwa
na umahiri wa watendaji wa RUWASA hasa katika utekelezaji wa Miradi mbalimbali
ya Maji katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri hiyo.
Kimsingi jukumu la Madiwani ni
kuhamasisha jamii kushiriki katika shughuli za maendeleo ikiwemo kuibua Miradi
ya maendeleo katika maeneo yao na kupatiwa taarifa namna Serikali inavyotoa fedha kwa ajili ya Miradi
mbalimbali pamoja na matumizi na ushirikishwaji wa wananchi katika kuilinda na
kuzuia uharibifu wa miundombinu.
Mkurugenzi huyo aliwataka wananchi
kuilinda miundombinu hiyo kwa sababu Miradi hiyo inafaida kwao na kwamba
Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan
imejikita kuhakikisha inamtua mama ndoo kichwani na kwamba wananchi wameshushudia
Miradi mingi ya maji ikitekelezwa kwenye Halmashauri hiyo.
“Lengo la Serikali kuweka Miradi
hiyo ni kwa ajili ya kuhakikisha inaboresha mazingira ya upatikanaji wa maji
kwa wananchi hivyo niwashauri wananchi muitunze Miundombinu hiyo ili iweze
kukaa muda mrefu na wananchi wanufaike na Miradi hiyo,hivyo ninyi waheshimiwa Madiwani
mnajukumu la kuhakikisha miundombinu ya Miradi yote ya maji inatunzwa na si
vinginevyo,” alisema Katimba.
Kikao cha Baraza la Madiwani wa
Halmashauri ya Msalala kilifanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri
hiyo huku Mkurugenzi huyo akitoa Onyo kali kwa wafugaji na kuwataka kuwa makini
na Mifugo yao ambayo imeelezwa kuwa ndiyo chanzo cha uharibifu wa Miundombinu
ya barabara katika maeneo mbalimbali nchini.
“Niwaombe sana ndugu zangu wafugaji,tuhakikishe
tunapitisha mifugo yetu katika maeneo maalumu yaliyotengwa wakati wa ujenzi,tuepuke
kupitisha mifugo kwenye barabara,lakini pia kwa upande wa wananchi wanaojishughulisha na shughuli za Kilimo tuache
kulima kandokando ya barabara zetu ninyi Madiwani hamasisheni ulinzi wa Miundombinu
hii muhimu ya maji pamoja na barabara,matumizi
sahihi ya Miundombinu hii yatatufanya tufanikiwe kunufaika katika Nyanja za Elimu, Maji
na Uchumi ” alisema Katimba.
Akizungumza na waandishi wa
Habari waliotaka kujua Siri ya mafanikio yaliyopelekea Wakala hiyo kupongezwa
na Madiwani wa Msalala Kaimu Meneja wa Wakala wa Maji Safi na Usafi wa
Mazingira Vijiji (RUWASA) Wilaya ya Kahama Pastory Mnyeti alisema kuwa,siku
hiyo baraza la Madiwani lilikaa kwa ajili ya bajeti kwa upande wa wadau kwa
maana ya RUWASA na TARURA ambao wamewasilisha kwa ujumla mpango na bajeti kwa
mwaka wa fedha 2024/2025.
Mnyeti alisema kuwa
mapendekezo ya bajeti yalifanyika kwa kushirikisha Madiwani ambao ndiyo wadau muhimu na ambao
ndiyo wanaokaa karibu zaidi na wananchi lakini pia ndiyo wanaojua mahitaji ya
wananchi wao hatua ambayo RUWASA imepongezwa na Madiwani hao kwa utekelezaji wa
Miradi ya maji katika maeneo yao.
“Sisi RUWASA bajeti yetu
imejikita katika Miradi inayoendelea,ili tuhakikishe inakamilika kwa wakati na kwamba
Miradi hiyo tuhakikishe inatoa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi kwa
wakati lakini pia kwa Miradi mipya pamoja na kuendelea kufanya Utafiti wa maji
chini ya Ardhi ili kuweza kupata vyanzo vipya vya maji kuongeza ufanisi katika
usimamizi wa Rasrimali za maji”alisema Kaimu Meneja huyo wa RUWASA.
Aidha Kaimu Meneja wa RUWASA
Pastory Mnyeti alimshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwapatia
fedha kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi bora ya maji lengo likiwa ni kuhakikisha
wanaondoa changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa
wananchi ili waweze kuendelea na shughuli zao za kiuchumi katika maeneo yao.
Kuhusu bajeti ya mwaka
2024/2025 Kaimu Meneja wa Wakala wa Maji safi na Usafi wa Mazingira Pastory
Mnyeti alisema kuwa wamependekeza kutumia kiasi cha shilingi Bilioni 10.2 ili
kupunguza changamoto katika maeneo yote ya Miradi iliyoainishwa na kwa Miradi
inayoendelea na kwamba kwa kipindi cha 2023/24 RUWASA ilitengewa kiasi cha
shilingi Bilioni 5.3 ambapo mpaka kufikia Disemba mwaka 2023 walipokea bilioni
2.7 na kwamba ndizo zinazoendelea kutumika mpaka sasa katika Miradi ya maji.
Naye Diwani wa Kata ya Mwakata
Siksi Ibrahimu alimtaka Kaimu Meneja wa RUWASA Pastory Mnyeti kuendelea
kujituma kwa kushirikisha Madiwani wa maeneo husika,huku akibainisha kuwa kiini
cha RUWASA kupongezwa na Madiwani kumetokana na maandalizi mazuri ya Taarifa
yake aliyoiandaa ambayo inaakisi uhalisia.
“Niwashukuru sana watendaji wa
Wakala wa maji safi na usafi wa Mazingira RUWASA sisi Madiwani kila mmoja wetu
amemsikiliza vizuri Kaimu Meneja,amezungumza vizuri na tumeelewa vizuri,Mhe.
Mwenyekiti mpaka muda huu wewe mwenyewe ni shahidi umewaona Madiwani
wameridhika na kikao kimetulia”alisema Diwani huyo.
Katika hali ambayo imezoeleka
ni kwamba mara nyingi katika Vikao kama hivyo Madiwani wasiporidhishwa na jambo
lolote hupaaza Sauti kupinga kinachosemwa na watendaji wa Serikali lakini kutokana
na taarifa ya Kaimu Meneja wa RUWASA Pastory Mnyeti,Madiwani wamekiri kuwa
taarifa hiyo imesheheni ukweli na hawana sababu ya kuikosoa wala kuipinga.
“Vikao kama hivi sisi Madiwani
tusiporidhishwa na jambo lolote huwa tunajipanga kupaaza Sauti kupinga
kinachosemwa na watendaji wa Serikali,lakini kutokana na taarifa ya Kaimu
Meneja wa RUWASA Madiwani wote tunakiri
kuwa taarifa hiyo imesheheni ukweli na
hatuna sababu ya kuikosoa wala kuipinga”alisema Mh Diwani huyo.
Chapisha Maoni