Top News

 


Waziri Mavunde Aagiza Jeshi la Polisi kutopelea Askari kulinda maeneo ya Leseni.











Pichani juu ni  Msafara wa Waziri wa Madini ukiwasili katika Ofisi za Mgodi wa  Utulivu Mining  na kupokelewa na wanakikundi wa kikundi hicho Picha na Anthony Sollo Nyanhwale.

NA ANTHONY SOLLO NYANHWALE.

WAZIRI wa Madini Anthony Mavunde amemuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi Mkoani Geita kutokubali kuombwa na kuwatoa Askari wa Jeshi hilo kwenda kulinda maeneo ya Leseni yanayoshikiliwa na baadhi ya Vigogo wanaotumia nguvu kubwa kuyalinda maeneo wanayoyashikilia kama Tegesha.

Akizungumza wakati wa kusikiliza malalamiko ya baadhi ya wanakikundi wa kikundi cha(Utulivu Mining Group)kilichopo Kijiji cha Bululu Halmashauri ya Msalala Mkoani Geita Waziri Mavunde amesema kuwa,mwenye jukumu la kulinda Leseni ni mmiliki wa Leseni mwenyewe.

“Serikali imeanza zoezi la kufuta Leseni za Utafiti na maombi ya Leseni yanayotegeshwa na watu,wapo watu wanaoshikilia maeneo makubwa sana bila kuyafanyia kazi,wanasubiri wachimbaji wadogo  wakikutana na mwamba  wanakimbilia Ofisi za Wakuu wa Wilaya kuomba Askari wa kwenda kuwatoa wachimbaji wadogo,niseme tu,huwezi kuwafanya wachimbaji wadogo kuwa watumwa katika nchi yao”alisema Waziri Mavunde.

Aidha Waziri Mavunde amesema kuwa,kutumia Ofisi ya Serikali ni kuigombanisha Serikali na wananchi wake,huku akisisitiza kuwa mwenye jukumu la kulinda Leseni ni Mmiliki wa Leseni.

“RPC msiwe mnawapeleka Askari katika mambo kama haya,kwa mujibu wa Sheria,jukumu la kwanza la mmiliki wa Leseni ni kulinda Leseni yake mwenyewe,lakini pia Leseni ya Utafiti ina Masharti yake,na moja ya masharti hayo ni kupeleka taarifa za Utafiti uliofanyika Ofisini kwa Waziri kila baada ya miezi mitatu”alisema Waziri Mavunde.

Katika hatua nyingine Waziri wa Madini Anthony Mavunde amewataka wawekezaji wa Kampuni ya Xin Tai Mining Company Limited kufanya  Utafiti na kuongeza thamani ya Madini kama Mkataba bainia ya pande mbili hizo unavyobainisha.

Hata hivyo kuhusu msaada wa kiufundi,Waziri wa Madini amesema Serikali iko mbioni kutoa utaratibu mpya juu ya msaada wa kiufundi(Technical Support) ili kuhakikisha Wawekezaji wanafanya shughuli zao bila kuvunja Sheria.

Baada ya kuupitia Mkataba ulioingiwa na pande mbili Kikundi cha Utulivu Mining na Kampuni ya  Xin Tai Mining Company Limited Waziri wa Madini,Anthony Mavunde amewataka wabia hao kutimiza Masharti ya Mkataba wa Ubia wa uwekezaji kwa kutoa msaada wa Kiufundi (Technical Support) kwa kikundi cha wachimbaji wadogo cha Utulivu Mining kilichopo Kijiji cha Bululu,Halmashauri ya  Nyangh’wale Mkoani Geita.

Aprili,2024 Waziri wa Madini Anthony Mavunde alifanya Ziara katika Kijiji cha Bululu Halmashauri ya Nyang'wale kwa lengo kukutana na wachimbaji hao na kufanya Mkutano nia ikiwa ni kutatua Mgogoro  uliokuwepo baina ya wanakikundi wachache kutoka kikundi cha Utulivu Mining na Mwekezaji wa Kampuni ya Xin Tai Mining Company Limited.

Kufuatia hali hiyo Waziri Mavunde alisema kuanzia sasa Serikali itaongeza umakini katika kuangalia Mikataba ya msaada wa Kifundi ili isiathiri malengo yaliyokusudiwa na Sheria.

Baada ya mazungumzo yaliyochukua takribani saa tatu,huku akizisikiliza pande zote mbili zinazohusika na mgogoro huo,Waziri Madini Anthony Mavunde alibaini kuwa katika Mkataba huo kulikuwa na kipengele cha utoaji wa msaada wa kiufundi kwa Kikundi cha Utulivu,ambao umeeleza bayana Masharti ambayo Mwekezaji kampuni ya Xin Tai anapaswa kutekeleza mara baada ya kusaini Mkataba huo.

"Sisi kama Wizara tunatekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye ametupa maelekezo mahsusi,kuhakikisha tunashughulikia masuala zikiwemo changamoto za wachimbaji wadogo ili nao wanufaike na rasilimali za nchi yao”alisema Waziri Mavunde.

Akielezea moja ya Masharti Waziri wa Madini Anthony Mavunde alieleza kuwa Sharti la kwanza kwa mwekezaji ni kuhakikisha anafanya Utafiti ikiwemo kuchoronga eneo lote la Leseni ya Kikundi cha Utulivu Mining ili kubaini mashapo ambayo yatapelekea kuongeza uzalishaji na hivyo manufaa kwa wachimbaji wadogo kama mkataba ulivyomtaka.

Katika hatua nyingine,Waziri Mavunde alimuagiza Mwekezaji kuhakikisha anatekeleza vipengele vya Mkataba kama unavyoeleza na kuhakikisha anapeleka Mitambo na Teknolojia ya kisasa kuwezesha uchimbaji katika eneo hilo,huku akisisitiza kwamba matarajio yake siyo kuendelea kuona Teknolojia na zana duni za wachimbaji wadogo zikizitumika na Mwekezaji.

 Waziri Mavunde alimuagiza mwekezaji pia kuhakikisha anaweka Mitambo ya kuongeza Thamani Madini atakayoyachimba kama Sharti la kimkataba linavyoeleza ili kuwasaidia wachimbaji wadogo katika maeneo yao.

Katika hali isiyo ya kawaida Waziri Madini Anthony Mavunde alikerwa na utaratibu wa utoaji wa msaada wa kiufundi kwa wachimbaji wadogo unavyotekelezwa kwa sasa, na kuahidi kwamba ataenda kutoa maelekezo Bungeni tarehe 30 Aprili, 2024 wakati atakapowasilisha bajeti ya Wizara ya Madini.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella alimpongeza Waziri Mavunde kwa namna ambavyo anashughulikia changamoto za wachimbaji wadogo na kuahidi kuwa Serikali ya Mkoa itaendelea kuunga mkono juhudi hizo za kuendeleza sekta ya Madini nchini.

Naye Mwenyekiti wa wachimbaji wadogo Wilaya Nyangh’wale Jeremiah Misana ameipongeza Serikali kwa kufuta Leseni na kuiomba kuwapa kipaumbele wachimbaji wadogo katika zoezi la ugawaji wa maeneo.

“Naipongeza Serikali kwa kufuta Leseni,lakini ombi langu lingine ni kwamba Serikali itoe kipaumbele kwa wachimbaji wadogo katika zoezi la ugawaji wa maeneo”alisema Misana.

 

 


Post a Comment

Mpya zaidi Nzee zaidi