NA ANTHONY SOLLO GEITA.
JAMII ya kundi la watu wenye ulemavu zaidi ya 700 kutoka Kata zote za Jimbo la Mbogwe Mkoani Geita kwa kauli moja wamempongeza Mbunge wa Jimbo hilo Nicodemus Henry Maganga kwa kuonyesha upendo kwao baada ya kuwakutanisha na kujadili changamoto mbalimbali zinazoikabili kundi la watu wenye Ulemavu Jimboni humo.
Kundi hilo lilikutana na Mbunge wa Jimbo Nicodemus Henry Maganga Julai 7 mwaka 2024 katika Ukumbi wa CASABLANCA ulioko Mji mdogo wa Masumbwe Halmashauri ya wilaya ya Mbogwe ambapo walipata fursa ya kueleza changamoto za kwa Mbunge huyo azipeleke Bungeni ili Serikali izifanyie kazi.
Licha ya Mbunge huyo kukutana na kundi la Jamii ya watu wenye ulemavu na kufanya majadiliano nao kwa saa kadhaa,Mbunge Maganga aliandaa chakula cha pamoja na lengo likiwa ni kusherehekea Siku ya Sabasaba ambayo ambayo imefikia kilele chake Kitaifa Julai 7 mwaka huu.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na wageni mbalimbali wakiongozwa na Mwanasheria wa Shirikisho la Vyama vya Wenye Ulemavu Taifa Wakili Msomi Gidion Mandesi,Mwenyekiti wa Chama cha Walemavu Wilaya ya Mbogwe Izengo Paul,Ofisa Ustawi wa jamii Mercy Joseph ambaye alikuwa akiwakilisha Viongozi wa Kitaifa ikiwemo Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe pamoja na Waziri wa Maendeleo ya Jamii jinsia wanawake na Makundi Maalumu.
Viongozi wengine waliohudhuria katika hafla hiyo ni pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Mashirika yasiyo ya kiserikali,Mashirika Jumuishi ya watu wenye Ulemavu Tanzania Bara kutoka Makao makuu Dodoma,Maofisa Ustawi ngazi ya Kata,Diwani wa Kata ya Nyakafuru Paul Edward Ngusa pamoja na Katibu wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Mbogwe Mheshimiwa Josephat Chacha.
Hata hivyo Watu wenye Ulemavu walimshukuru Mbunge wa jimbo la Mbogwe Nicodemus Maganga kwa kuwajali watu wa kundi hilo ambalo walisema limesahaulika muda mrefu huku wakiiomba Serikali kuwakumbuka katika nafasi mbalimbali za Uteuzi na Ajira.
"Tunamshukuru sana Mbunge wetu Mheshimiwa Nicodemus Maganga kwa kutuunganisha sisi jamii ya watu wenye ulemavu tunaoishi Wilaya ya Mbogwe na Mashirika na Taasisi mbalimbali za Kitaifa na watu wenye Ulemavu,ametualika na kutugharimia nauli,jambo hili ni kubwa na sisi tunamuahidi kuwa tuko pamoja naye katika safari ya kutimiza ndoto zake za kuendelea kuwa Mbunge wa jimbo letu la Mbogwe"alisema Katibu Izengo.
Katika hatua nyingine,Jamii ya watu wenye Ulemavu wamewashukuru Viongozi wa Wilaya ya Mbogwe akiwemo Mkuu wa Wilaya Bi Sakina Mohamed,Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbogwe kwa kuendelea kuhudumia jamii ya watu wenye Ulemavu katika Halmashauri hiyo.
"Sisi kama Jamii ya watu wenye Ulemavu tunawashukuru Viongozi wa Wilaya ya Mbogwe akiwemo Mkuu wa Wilaya Bi Sakina Mohamed, Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe Bi Saada Mwaruka kwa kuendelea kutuhudumia sisi jamii ya watu wenye Ulemavu katika Halmashauri hii,tukiri wazi wametutendea Haki,na ombi letu tunaomba Serikali itusaidie kupata Mikopo ili tuweze kufanya Shughuli zetu za kujiongezea kipato"ilisema sehemu ya Risala kwa Mgeni Rasmi.
Hata hivyo Jamii ya watu wenye Ulemavu kutoka Halmashauri ya wilaya ya Mbogwe wametoa mapendekezo kwa Serikali ya Halmashauri ya wilaya ya Mbogwe kufikisha Kliniki ya Watu wenye Ulemavu wa Ngozi Albino katika Kituo cha Afya Masumbwe ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za Madawa na mafuta yanayotumika kwa watu wenye ulemavu wa ngozi Albino.
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la
Mbogwe Mkoani Geita Mheshimiwa Nicodemus Henry Maganga ameahidi kufanya Ziara
katika Vijiji 30 ili kukutana na Makundi ya watu wenye Ulemavu na kusikiliza changamoto
zao ni kuzitafutia ufumbuzi ikiwemo kuzifikisha katika Ofisi za Bunge ili
ziweze kuboreshwa kwa maslahi ya watu wenye Ulemavu.
"Ndugu zangu wenye ulemavu nimesikiliza changamoto zenu,hivi karibuni natarajia kufanya Ziara katika Vijiji 30 ili kukutana na Makundi ya watu wenye Ulemavu na kusikiliza changamoto zenu na kuzitafutia ufumbuzi ikiwemo kuzifikisha katika Ofisi za Bunge ili Serikali iweze kuboresha kwa maslahi ya watu wenye Ulemavu"alisema Maganga.

Chapisha Maoni