NA ANTHONY SOLLO GEITA.WAKATI siku za Kampeni za kuwaombea Kura Wagombea wa nafasi za uongozi kwa Vyama mbalimbali katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa zikielekea ukingoni,Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameendelea kuwaombea kura
Wagombea wa Chama cha Mapinduzi na kuwahimiza wananchi kuwachagua ili kuendeleza Miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Wilaya yao.
Akihutubia katika Mkutano wa Kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa zilizofanyika Novemba 23,2024 katika Viwanja vya Shule ya Msingi Bwanga Wilaya ya Chato Mkoani Geita,Dkt. Biteko amesema
kuwa CCM ina nia ya kuendelea kuleta maendeleo na akivitaka Vyama vingine vishindane kwa hoja badala ya matusi huku akiwataka wanasiasa kuwaunganisha
Watanzania badala ya kuwagawa kwa Itikadi za Vyama vyao.
"Ndugu zangu niwaombe sana,wasikilizeni na wagombea wa Vyama vingine lakini msifanye kosa kwa kuwachagua maana wanataka Vyeo tu, msikubali kuwapigia kura watu wanaowaambia mkunje ngumi,hawana Ilani iliyopitishwa na wananchi wala bajeti wanataka muwachague wakafanye kazi gani?,”amehoji Dkt. Biteko.
Aidha Dkt Biteko amesema kuwa katika Uchaguzi wa Mwaka 2024, CCM imejipanga kushinda na si kubahatisha kwani mipango yake imeanzia kwa wanachama wake kujitokeza kwa wingi katika hatua za awali kwenye uandikishaji wa Daftari la wapiga kura kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Kwa mujibu wa Dkt Biteko katika Wilaya ya Chato Idadi ya waliojiandikisha kwenye Daftari la wapiga kura walifika zaidi ya 200,000 na bila ya shaka wataenda kupiga kura, CCM ina uwezo wa kuleta maendeleo kwenye Wilaya yenu, Viongozi watakaochaguliwa wataenda kufanya kazi kwa sababu ilani ipo, CCM tuna ilani na mipango!!wengine hawana,” ameeleza Dkt. Biteko.

Dkt Biteko pia amesema kuwa tangu Rais Samia aingie Madarakani CCM imekuwa na kauli mbiu ya "kazi iendelee" huku ikiendeleza kwa juhudi kubwa Miradi ya maendeleo kwa maslahi ya Nchi .
Naibu Waziri Mkuu huyo ameitaja Miradi hiyo kuwa ni pamoja na Mradi wa kufua wa Umeme wa Bwawa la Julius Nyerere ambao sasa unafanya kazi, Treni ya Umeme ya kisasa (SGR)amvayo nayo inafanya kazi kutoka Dar es salaam hadi Dodoma, uimarishaji wa Shirika la Ndege kwa kuongeza Udadi ya Ndege.
Katika hatua nyingine Dkt. Biteko amesema kuwa CCM inaheshimu Uchaguzi wa Serikali Mtaa na ndio maana viongozi wake wote wa ngazi za juu wamesambaa katika maeneo mbalimbali kueleza umuhimu wa Uchaguzi huo.
“ Sisi kama Chama cha Mapinduzi tuna kila sababu za kuomba kura hii ni kutokana na kwamba tumefanya kazi inayoonekana, niwaombe wana Chato Nov 27 mwaka huu tukapige kura kuchagua wagombea wa CCM katika ngazi za Vitongoji na Vijiji hakuna kumwachia mtu kwa kuwa wengine hawana Ilani wala mipango,” amesema Dkt. Biteko.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Chato, Dkt. Medard Kalemani amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuipelekea fedha Halmashauri ya Wilaya ya Chato.
Aidha akizungumzia fedha za Miradi ya Maendeleo Mbunge wa Jimbo la Chato Dkt Kalemani amebainisha kwamba katika kipindi cha Uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan Wilaya ya Chato imepata Sh bil 197.28 kwa ajili ya kuendeleza Miradi ya maendeleo.
“Tumepata Sh Mil 100 kwa ajili ya kujenga kituo cha Mabasi, na kwa upande wa Kituo cha Afya Rais Samia ametupatia fedha kwa ajili ya kufanya ukarabati,”
Mbunge huyo pia amesema kuwa awali Bwanga kulikuwa na shida ya umeme tunakushukuru kwa sasa umeme umefika katika vitongoji na vijiji 15.
"Nataka nikuhakikishie,fedha tulizopata za Miradi mikubwa kumi ikiwemo Mradi wa uwanja wa Ndege ambao unaendelea vizuri ndege zinatua, ujenzi wa Chuo Kikuu cha Mipango na Fedha kimekamilika na mwezi ujao kinafunguliwa, ujenzi wa Maktaba ya Kanda Miradi inayogharimu Sh bil 7.2 ambayo tayari imeshaezekwa.
Dkt Biteko amewahimiza wananchi wa Bwanga kuchagua wagombea wa CCM katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili kuendeleza maendeleo Bwanga na Chato kwa ujumla
Chapisha Maoni