Hotuba ya Naibu Waziri Mkuu Dkt Biteko yaufilisi Upinzani,Asema CCM Inaeleza Hoja,Wao wanahimiza watu kukunja Ngumi.
Awataka Wananchi Kuchagua Viongozi Watakaotatua changamoto zao.

NA ANTHONY SOLLO MBOGWE.
MBUNGE wa Jimbo la Bukombe ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Mashaka Biteko amewataka wananchi kuchagua Wagombea wa CCM kwa kuwa hoja zao zinatekelezeka kutokana na kazi zilizotekelezwa kupitia Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
Dkt Biteko ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa amesema hayo leo Novemba 22,2024 wakati akifungua Kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa zilizofanyika katika Viwanja vya Shule ya Lulembela iliyoko katika Kata ya Lulembela Halnashauri ya Wilaya ya Mbogwe Mkoani Geita.

Aidha Naibu Waziri Mkuu Dkt Biteko amesema awali katika Wilaya ya Mbogwe haikuwa na Shule za Sekondari, Zahanati,Vituo vya Afya na kwamba hata watoto walikuwa wakifaulu na wanakosa Shule ya kuwapeleka, lakini kutokana na jitihada zilizofanywa na CCM sasa Wilaya ya Mbogwe imekuwa na Maendeleo makubwa ikiwemo Miradi ya maji,barabara na umeme.
Hata hivyo Dkt Biteko amewahimiza wananchi kuchagua wagombea wa CCM, ili kuwa na Safu nzuri ya Uongozi iliyojengwa Imara kutoka chini hadi juu ili kurahisisha utekelezaji wa Miradi ya maendeleo.
Kuhusu Ushindi Dkt Biteko alisisitiza kuwa ushindi ni mipango na Chama cha Mapinduzi tayari kimejipanga na kuhamasisha wanachama na wananchi kujiandikisha na kushiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, na kuwataka wana CCM kutembea kifua mbele kwa kuwa Chama kinatambua mahitaji ya wananchi na kiko tayari kuyatekeleza.
“Nataka niwaombe wananchi wote twende tukachague Wagombea wa CCM ambao watashughulika na shida zenu, na niwaambie,CCM haitaki ushindi wa kubebwa, tunataka ushindi halali na sababu ya ushindi halali tunayo kwa kuwa tumetekeleza Miradi mingi ya maendeleo kwa wananchi, tulihamasisha kwa wingi watu wetu kujiandikisha na tunaamini mtajitokeza kupiga kura Novemba 27, 2024,” amesema Dkt. Biteko.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mbogwe, Mhe. Nicodemas Maganga amesema kuwa CCM wataomba kura kistaarabu na kuwahimiza wananchi kuchagua wagombea wa CCM ifikapo Novemba 27, 2024.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Mkoa wa Geita, Mhe. Rose Busiga amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia Halmashauri ya Mbogwe fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa Miradi mbalimbali katika Wilaya za Mkoa wa Geita.
Busiga ametaja baadhi ya Miradi huku akisema kuwa Asilimia 100 ya Vijiji vyote Mkoani Geita vina Nishati ya Umeme na tayari Serikali imeendelea kutekeleza Miradi ya Barabara, Zahanati,Hospitali na Shule.
Katika hatua nyingine Mbunge huyo wa Viti Maalumu Mkoa wa Geita amewahamasisha wananchi wa Mbogwe kuchagua wagombea wa CCM katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kumchagua Rais Samia katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2025.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Mbogwe, Mathias Nyororo amesema kuwa katika Vitongoji 335 vilivyopo katika Wilaya ya Mbogwe Vyama vingine vimeweka wagombea katika Vitongoji 14, huku katika Vijiji 87 wameweka wagombea 17 pekee.

Chapisha Maoni