
NA ANTHONY SOLLO MOROGORO.
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi amewaelekeza Watumishi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori TAWA kuendelea na matumizi ya Teknolojia mbalimbali katika ulinzi wa rasilimali ya Wanyamapori.
Dkt. Abbasi ametoa maelekezo hayo Disemba 10, 2024, katika Kikao chake na watumishi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) ambacho kilichofanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya TAWA Mkoani Morogoro.
"Niwaombe tuendelee kutumia Teknolojia za kisasa katika ulinzi wa rasilimali ya wanyamapori ", alisema Dkt. Abbasi.
Dkt. Abbasi ameipongeza TAWA kwa utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa katika ziara yake ya kikazi Mkoani Ruvuma mnamo mwezi Septemba ya kununua ndege nyuki kwa ajili kudhibiti wanyama wakali na waharibifu.

"Nimefurahi kuona mmeanza kutekeleza maelekezo ya Rais ya kununua ndege nyuki,hapa TAWA nimeona kazi imeanza" alisema Dkt. Abbasi
Hata hivyo Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbasi aliwapongeza TAWA kwa ujenzi wa vizimba sambamba na ujenzi wa mabwawa katika Hifadhi ya Rungwa na Makuyuni ambao utasaidia kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji kwa wanyamapori.
Kwa upande wake,mwakilishi wa Kamishna wa Uhifadhi TAWA, Kaimu Naibu Kamishna wa Uhifadhi, Mlage Kabange alimshukuru Katibu Mkuu kwa ujio wake na kusema kuwa,maelekezo yaliyotolewa yatatekelezwa kwa wakati.

" Sisi kama TAWA ni kawaida yetu kupokea maelekezo na kuyafanyia kazi bila kupindisha" alisema Kamishna Mlage Kabange.
Akizungumzia matumizi ya Teknolojia, Kamishna Kabange alikiri kuwa TAWA imenunua ndege nyuki 11 kwa ajili ya shughuli za Uhifadhi na itaongeza nyingine zaidi, ikiwa ni pamoja na kutafuta teknolojia zingine zitakazosaidia katika shughuli za Uhifadhi.

Dkt.Abbasi alipata muda wa kuangalia Onesho la Matumizi ya Ndege Nyuki zikitumika kumrudisha Tembo hifadhini sambamba na kukabidhiwa kombe la SHIMMUTA kutokana na mashindano ya Kamba na Riadha.



Chapisha Maoni