NA ANTHONY SOLLO BUNGENI DODOMA
WAKATI Wachimbaji wadogo wakilia na utitiri wa Tozo katika Mnyororo wa Uchimbaji wa Madini,Mbunge wa Jimbo la Busanda Mh Tumaini Bryceson Magessa ameuliza swali kwa Waziri wa Madini akitaka kujua ni lini Serikali itapitia upya Tozo zilizopo kwenye mnyororo wa uchimbaji na uchenjuaji wa Madini ya Dhahabu ambazo zimekuwa ni Kero kwa Wachimbaji Wadogo.

“Je, lini Serikali itapitia upya Tozo zilizopo kwenye mnyororo wa uchimbaji na uchenjuaji wa Madini ya Dhahabuzinazowaelemea Wachimbaji Wadogo”?
Akijibu swali hilo,Waziri wa Madini amesema,Wizara kupitia Mkakati wa Kuboresha Mazingira ya Biashara nchini (MKUMBI) imefanya Utafiti wa Tozo 66 zinazotozwa na Halmashauri katika shughuli za madini ikiwemo Madini ya Dhahabu,Tozo zilizobainika katika shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa dhahabu ni pamoja na ushuru wa karasha, Ada ya ukaguzi, Vat leaching/CIP,Mialo,Ushuru wa kusafirisha miamba ya Madini (mbale) na visusi (mabaki ya miamba baada ya kuchenjuliwa (tailings).
Aidha Waziri wa Madini Anthony Mavunde ameliambia Bunge kuwa,katika kutatua changamoto hizi,Wizara iliitisha kikao Mwezi Agosti, 2024 Mkoani Singida ambacho kilishirikisha Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Wizara ya Fedha,Tume ya Madini, STAMICO, Halmashauri za Wilaya(Ikungi,Chunya,Kahama,Msalala,Meatu, Shinyanga,Mtama na Lindi), FEMATA na TAWOMA.
Waziri Mavunde amesema kuwa, rasimu ya Mapendekezo ya Maboresho tayari imeshaandaliwa na ipo katika hatua ya kufanyiwa mapitio na tathmini, ambapo Matokeo ya tathmini hiyo yatatusaidia katika kupanga tozo rafiki kwa wachimbaji wadogo.

“Mheshimiwa Spika,kutokana na changamoto za kikodi nchini,Mheshimiwa Rais ameunda Tume ya Maboresho ya Kodi ili ifanye tathmini ya mfumo wa kodi na kuleta mapendekezo ya namna ya kuboresha mfumo wa kodi ni imani yetu kuwa maboresho hayo yataangazia changamoto za kikodi zinaziikabili Sekta ya Madini”anasema Waziri Mavunde.
Chapisha Maoni